Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeshiriki katika Mkutano wa Mawaziri wa Biashara wa Nchi za Jumuiya ya Madola (JYM) na Kongamano la biashara kwa Nchi za Jumuiya ya Madola unaofanyika Windoek, Namibia tarehe 16 hadi 20 Juni 2025 na kuongozwa na Mhe. Selma Shipala-Musavyi (MB), Waziri wa Biashara wa Namibia.
Mkutano huu umeleta pamoja Mawaziri wa Viwanda, Wafanyabiashara na Wabunifu nchi za JYM kwa lengo la kujadili fursa za ushirikiano katika biashara na uwekezaji.
Aidha mkutano huu ulitangaliwa na Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Biashara, Senior Trade Officials Meeting (STOM) uliofanyika Windhoek, tarehe 16 hadi 17 Juni 2025. Pembezoni na mwa Mkutano huo, pia umefanyika Commonwealth Business Summit, tarehe 18 hadi 20 Juni 2025 itakayoratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola.
Kwa mara ya kwanza, mkutano huu wa Mawaziri wa Biashara wa Jumuiya ya Madola unafanyika barani Afrika, katika kipindi muhimu sana.
Mawaziri wamekusanyika wakati ambapo sera za kujilinda kibiashara, mvutano wa kisiasa wa kimataifa, na ushuru mpya vinaendelea kuibadilisha taswira ya biashara ya dunia. Kwa mataifa mengi ya Jumuiya ya Madola, hasa yale madogo na yaliyo hatarini zaidi, hatari zinazidi kuongezeka.