Thursday, July 17, 2025

20 wauawa katika msongamano eneo la misaada la Gaza

Share

Watu 20 waliokuwa wakijaribu kupata chakula wameuawa “kufuatia machafuko na ongezeko la hatari” katika kituo cha usambazaji wa misaada kusini mwa Gaza, Shirika la Kibinadamu la Gaza linaloungwa mkono na Marekani na Israel (GHF) linasema.

Kumi na tisa walikanyagwa hadi kufa na mmoja alidungwa kisu katika “tukio hilo la kusikitisha” katika eneo la GHF katika eneo la Khan Younis, taarifa ilisema, ikiongeza kuwa inaamini kuwa wimbi hilo “liliendeshwa na waasi katika umati” ambao walikuwa washirika wa Hamas.

Haikuwezekana mara moja kuthibitisha ripoti hiyo. Hata hivyo, Hospitali ya Nasser iliyoko Khan Younis hapo awali ilisema kuwa imepokea miili ya watu 10 waliouawa kutokana na “kukosa hewa” baada ya kituo cha msaada kufungwa na wakandarasi binafsi wa usalama wa GHF wa Marekani.

Kumekuwa na ripoti karibu kila siku za Wapalestina kuuawa walipokuwa wakitafuta msaada tangu GHF ilipoanza operesheni mwishoni mwa mwezi Mei.

Mashahidi wanasema wengi wamepigwa risasi na wanajeshi wa Israel. Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema Jumanne kuwa hadi sasa imerekodi mauaji 674 katika maeneo manne ya GHF kusini na katikati mwa Gaza katika muda wa wiki sita zilizopita.

Mauaji mengine 201 yamerekodiwa kwenye njia za Umoja wa Mataifa na misafara mingine ya misaada, iliongeza.

Chanzo: BBC Swahili

Table of contents [hide]

Read more

Local News