Geita yafikia 95% utekelezaji wa ilani ya CCM

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakiwa kwenye kikao Cha baraza la madiniwani

HALMASHAURI ya wilaya ya Geita mkoani hapa imeweka wazi kuwa mpaka kufikia Februari 2025 tayari imefikia asilimia 95 ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, Khadija Said amesema hayo katika mkutano wa Baraza la Madiwani kwa Kipindi cha Robo ya Pili kwa mwaka wa Fedha 2024/25.

Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano kati ya madiwani, viongozi na maofisa wa halmashauri ambapo kila mmoja kwa nafasi yake amewajibika kikamirifu kutatua kero za wananchi.

Amesema kupitia fedha zinazotolewa na serikali ya awamu ya sita halmashauri imesimamia kwa uafasaha kuhakikisha kila kata, kijiji na kitongoji kinapata huduma muhimu za kijamii hususani maji, afya na elimu.

“Kama kuna diwani ambaye ameshindwa kutekeleza ahadi alizotoa kwenye kata yake, nitoe wito kwa madiwani wenzangu waendelee kukumbuka zile ahadi alizotoa ili waweze kuondoa adha za wananchi”, amesema.

Diwani wa Kata ya Bukoli, Faraji Self amesema kwa upande wa kata hiyo utekelezaji wa ilani umefikia asilimia 93 na juhudi kubwa zinafanyika ili kukamilisha asilimia 100 kabla ya kuvunjwa kwa bunge.

Faraji amedokeza miradi inayoendelea ni ujenzi wa jengo la upasuaji, jengo la zahanati na maabara katika kijiji cha Ntono pamoja na shule mpya ya sekondari.

“Changamoto kubwa iliyopo ni mfumo wa NEST, ambao ndio unatusumbua lakini watendaji tunawapongeza kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya kwenye miradi hii hakuna hujuma”, amesema

Diwani wa kata ya Busanda, Seleman Gamala amesema ndani ya miaka minne kata hiyo imepokea zaidi ya sh billioni mbili kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali sambamba na pesa za mfuko wa jimbo.

“Kata ya Busanda mfuko wa jimbo umetunufaisha sana, tumepokea zaidi ya sh milioni 22 kwa ajili ya ujenzi wa daraja, ofisi za kijiji, mara ya kwanza tulipokea milioni 18, mara ya pili tukapata milioni nne.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Exit mobile version