Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), taendelea kuweka kipaumbele katika kufanya uchunguzi wa ajali za barabarani ili kubaini visababishi vya ajali hizo hatua ambayo itasaidia juhudi za mamlaka hiyo na wadau kwa ujumla za kuweka mkakati wa kupunguza ajali hizo
Hayo yameelezwa Jijini Dar es Salaam, na Meneja Uratibu Usalama na Mazingira – LATRA, Bw. Geoffrey Silanda, wakati wa kikao cha Wadau wa Usalama Barabarani kilichofanyika ofisi za Mamlaka hiyo zilizoko Mtaa wa Nkurumah, Alhamisi ya Aprili 17, 2025
Katika kikao hicho, ripoti kadhaa za ajali za barabarani zilizotokea hivi karibuni, ziliwasilishwa ambapo wadau waliweza kujadili kwa kina kuhusu taarifa hizo sanjari na kutoa mapendekezo kadhaa ambayo wadau wamesema kama yatafanyiwa kazi matukio ya ajali yatapungua na hivyo kuokoa uhai wa watumia barabara nchini
Bw. Silanda amesema imedhamiria kuendelea kufanya chunguzi za ajali mbalimbali nchini ni kubaini vyanzo vya ajali hizo na kutafuta njia ambazo zitatumika kuzuia ajali za namna hiyo zisitokee tena.
Naye ACP Joseph Mwakabonga, Mkuu wa Operesheni Kikosi cha Usalama Barabarani, amesema kikao hicho kinasaidia kupata suluhisho la tatizo la ajali za barabarani kwani mada mbalimbali zilizojadiliwa katika kikao hicho ni wazi kuwa utekelezaji wake utasaidia kupunguza ajali nchini.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani, Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TAMSOA), Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Chuo cha Taifa za Usafirishaji (NIT) na Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA)