Karibu asilimia 55 ya taarifa za vifo vinavyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi nchini (WCF) ni zile zinazoonyesha kuwa chanzo chake ni ajali za barabarani, takwimu zinazoashiria kuwa ajali hizo ni janga lenye kugharimu nguvu kazi ya taifa.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini wa WCF, Dkt. Abdulssalaam Omar, katika hafla fupi ya kuhitimisha maadhimisho ya nane ya Wiki ya Kimataifa ya Usalama Barabarani iliyoandaliwa na asasi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA Tanzania) na kufadhiliwa na mfuko huo pamoja na Shirika la Kimataifa la Global Alliance.
Akiongea mbele ya Mabalozi waliohudhuria hafla hiyo, Dkt. Omar amesema, takwimu hizo mbali ya kudhoofisha nguvu kazi katika kukuza uchumi wa nchi, zinaonyesha ni kwa kiasi gani mfuko huo unatakiwa kuwekeza katika kushirikiana na wadau kwenye jitihada za kuimarisha usalama barabarani nchini.
“Ushiriki wetu katika tukio hili unaendelea kuonyesha azma ya WCF ya kuimarisha na kuendeleza ushirikiano wetu na wadau katika kuhakikisha elimu ya usalama barabarani inafika kwa watumiaji wote wa barabara pamoja na kuhamasisha watumia barabara hao kupaza sauti ili kwa pamoja tutokomeze ajali hizi ambazo ni mzigo kwa taifa letu” amesema Dkt. Omar.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa huduma za Tathmini wa WCF, ameendelea kusisitiza wafanyakazi wanaopata ajali wakiwa njiani kwenda au kutoka makazini au wakiwa katika safari za kikazi, kuhakikisha wanawasiliana na mfuko huo, kwani hao ni wenye kustahili kulipwa fidia kupitia mfuko huo.
Akiongea katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa RSA Tanzania balozi Augustus Fungo amesema, Shirika linajivunia kuwa asasi kinara katika harakati za kuimarisha usalama barabarani nchini kupitia programu mbalimbali za uelimishaji, ukemeaji na utoaji taarifa za changamoto za barabarani, na kuwashukuru wadau wote ambao wamekuwa wakijitokeza kuunga mkono juhudi hizo wanazozifanya.
“Asasi hii inaundwa na watu ambao wanajitolea kwa zaidi ya asilimia 90, wakijitolea muda na gharama zao ili kutekeleza programu za taasisi, licha ya uhaba wa vitendea kazi kama vipeperushi kwa ajili ya uelimishaji na hata kufanya machapisho mengine yenye lengo la kuelimisha na tunaomba wadau waendelee kutuunga mkono kwa kuwa usalama barabarani ni jukumu letu sote.
Maadhimishi ya nane ya Wiki ya Kimataifa ya Usalama Barabarani 2025, yalibeba ujumbe wa Tuimarishe Usalama wa Watembea kwa Miguu na Waendesha Baiskeli, ujumbe ambao umelenga kuhamasisha mamlaka zinazohusika na usanifu na ujenzi wa barabara kuhakikisha zinajumuisha miundombinu kwa ajili ya kundi hilo la watumia barabara, ambalo limekuwa likiathiriwa zaidi na matukio ya ajali za kugongwa na vyombo vya moto.