
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, amewataka wana-CCM kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushika dola katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama inavyoelezwa katika Katiba ya CCM.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Miaka 48 ya CCM, yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma. Alipongeza viongozi, wanachama, na wapenzi wa CCM kwa mafanikio makubwa yaliyojiri katika kipindi hicho cha miaka 48.
“Kwa hakika, wana-CCM tunayo kila sababu ya kufurahi na kujivunia mafanikio makubwa ambayo chama chetu kimeyapata. Sote tunawajibika kuyadumisha mafanikio haya kwa kuimarisha umoja na mshikamano. Tunakabiliwa na uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha chama chetu kinaendelea kushika dola,” alisema Dk. Mwinyi.
Aidha, Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kuwaandikisha wanachama wote katika daftari la wapiga kura na kuwahamasisha kwenda kupiga kura wakati wa uchaguzi, ili kuhakikisha CCM inashinda na kuendelea kushika dola.