
Hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kusaini agizo la kuiondoa nchi hiyo katika Shirika la Afya Duniani (WHO) siku chache zilizopita imeanza kuleta athari kadhaa hususan barani Afrika kama ilivyokuwa ikitarajiwa.
Licha ya kuwa kuna sheria zinazohitajika kufuatwa kwa taifa linalotaka kundoa ufadhili wake, Utawala wa kiongozi huyo mpya tayari umechukua hatua ya kusitisha usambazaji wa dawa za kuokoa maisha za HIV, Malaria na Kifua kikuu mbali na dawa za watoto wachanga katika mataifa yote yanayosaidiwa na shirika la USAID duniani, kulingana na barua iliopatikana na vyombo vya habari.
Athari hizo zinatokana na Marekani kuwa mchangiaji mkubwa wa kifedha wa WHO na programu mbali mbali zilizopo chini ya shirika hilo na taasisi nyingine kubwa za kiafya duniani.
Hatua hii imepokelewa vipi?
Siku ya Jumanne juma lililopita, wakandarasi na washirika wanaofanya kazi na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) nchini Tanzania na Kenya walianza kupokea barua hizo ili kusitisha ufadhili huo mara moja, kulingana na vyanzo.
Tanzania nchi ambayo ilikuwa ikifaidika na misaada hiyo, amri hiyo ya Rais Trump mbali na kuathiri sekta ya Afya, pia inaweka hatarini ajira za watu.
Johansen Josephat, Afisa Mawasiliano Kutoka Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na uboreshaji wa huduma ya afya kwa umma nchini Tanzania ametoa maoni yake kwa kueleza jinsi walivyoguswa.
Johansen akizungumza na BBC anasema hatua hii imekuwa pigo lakini wanajaribu kushirikiana na serikali kuangalia kwa namna moja au nyingine kuhakikisha kwa namna gani wanaendelea kutoa nguvu au mchango katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
”Ukiangalia kuna maelfu ya watanzania ambao tayari wana hii changamoto ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi wanaotumia dawa, kwahiyo sisi kama wadau wa serikali tumekuwa kama mkono wa pili wa serikali, kusititishwa huku kwa ufadhili kutoka Marekani kunakwenda moja kwa moja kwa wale waajiriwa walioko vituoni,.ni kwamba zile huduma vituoni zitarudi.
Sababu za kusitishwa kwa ufadhili
Trump ni mkosoaji wa muda mrefu wa Marekani kutumia fedha zake kufadhili mataifa mengine akisema hauwakilishi thamani kwa kodi wanazotoa Wamarekani.
Amekosoa vikali USAID, akielezea viongozi wake wa juu kama “watu wasiojielewa .”
Kufunga shirika hili kutaweza kupigiwa upatu kutoka kwa Wamarekani.
Tafiti za maoni kwa muda mrefu zimeonesha kuwa wapiga kura wa Marekani wanapendelea serikali yao kupunguza matumizi ya misaada ya kigeni.
Kwa mfano, moja ya hatua za kwanza alizochukua Trump alipochaguliwa tena ilikuwa kusaini amri ya kiutendaji inayohusisha kusitisha takribani matumizi yote ya kimataifa kwa muda wa siku 90 ili kupitia upya matumizi hayo.
Notisi ikatolewa ikisitisha shughuli zinazoendelea zisimamishwe mara moja.
Muda mchache baadaye agizo likatolewa kuwa baadhi ya programu za kibinadamu ziendelee, ingawa agizo la awali lilikuwa limevuruga shughuli kadhaa kote ulimwenguni.
‘Ni pigo lakini tunatafuta ufumbuzi’
Johansen amekiri kuwa amri ya Trump ni pigo lakini ‘tunajaribu kushirikiana na serikali kuangalia kwa namna moja au nyingine, tunahakikisha kwa namna gani tunaendelea kutoa nguvu au mchango katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI’, Alisema.
”Ukiangalia kuna maelfu ya watanzania ambao tayari wana hii changamoto ya maambukizi ya Virusi wanaotumia dawa, kwahiyo sisi kama wadau wa serikali tumekuwa kama mkono wa pili wa serikali,kusititishwa huku kwa ufadhili kutoka Marekani kunakwenda moja kwa moja kwa wale waajiriwa walioko vituoni.”
Hatua hii imeathiri kiasi gani?
Moja kati ya miradi inayohudumiwa na watu wengi,ni miongoni mwa iliyoathirika kufuatia kufungwa kwa ufadhili wa marekani barani Afrika kupitia CDC.
Idadi kubwa ya wafanyakazi wa shirika la misaada MDH wapo ktk siutafahamu wakisubiri kujua hatma ya ajira zao wakati huu mashirika ya misaada ambayo yamekuwa yakiendeshwa kwa ufadhili wa serikali ya Marekani yakiwa yamefungwa.
”Sisi ni Watanzania na miongoni mwetu ni walengwa wa hili tutaendelea kujitolea kufanya kazi za utoaji wa huduma elimu na dawa kwa wanaoishi na changamoto ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa kupitia manispaa zetu.
”Tukisema tunasubiri mfadhili wakati tuna watu wanaoishi kwa kutegemea hizi dawa,tuliamua kuendelea kutoa huduma bila kujali maslahi”, Alisema Johansen.
Chanzo: BBC Swahili