
Akizungumza kuhusu uwepo wa wanajeshi wa Afrika kusini katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo Rais Cyril Ramaphosa, alisema watafanya kazi “ili wanajeshi wetu wanarudi nyumbani”.
Katika hotuba yake kwa taifa jana usiku, Ramaphosa – ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo kubwa nchini mwake kwa siku kadhaa baada ya wanajeshi 14 wa nchi yake kuuawa katika mapigano katika wiki za hivi karibuni DRC- alisema suluhu la amani lazima lipatikane.
Afrika Kusini imetuma zaidi ya wanajeshi 1,000 katika kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kusaidia jeshi la DRC kupambana na waasi wa M23.
Alisema: “Tunatoa wito kwa pande zote kuafiki juhudi za kidiplomasia zinazoendelea za kutafuta suluhu la amani, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mazungumzo ya Luanda.”
Amethibitisha kuwa atahudhuria mkutano wa wakuu wa EAC na SADC unaoanza Ijumaa hii na kumalizika kesho Jumamosi, jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Kuhusu mkutano wa Dar es Salaam, Ramaphosa alisema: “Tutasisitiza wito wetu wa kusitishwa kwa uhasama na kuanza tena mazungumzo ili kufikia suluhu la kweli na la kudumu, na tutajitahidi kuhakikisha wananajeshi wetu wanarejea nyumbani.”
Baadhi ya wabunge wa bunge la Afrika Kusini wiki hii walilaani uamuzi wa nchi hiyo kutuma wanajeshi wake DR Congo, na kwamba Wizara ya Ulinzi bado haijapata miili ya wanajeshi waliouawa huko.
Afrika Kusini, Malawi na Tanzania ni nchi za SADC ambazo zimetuma wanajeshi kuisaidia serikali ya DR Congo. Siku ya Jumatano, Rais wa Malawi alitangaza kwamba jeshi la nchi yake linapaswa kujiandaa kurejea nyumbani.
Chanzo: BBC Swahili