
DAKTARI Bingwa wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu kutoka Chama cha Wataalmu wa Kifafa Tanzania, Dk Patience Njenje amesema imani za kishirikina zimekuwa zikigharimu maisha ya wagonjwa wa kifafa kwa kukabiliwa na unyanyapaa ambapo asilimia 50 ya jamii inaamini kuwa kifafa kinaambukiza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam ikiwa ni wiki ya maadhimisho ya kifafa Februari 3 hadi 9 na kuelekea siku ya kifafa Duniani Februari 10 dk Njenje amebainisha kuwa utafiti pia umeonesha kuna takribani watu milioni moja wanaoishi na kifafa nchini.
“Watoto wanaougua kifafa wenye umri wa kwenda shule asilimia 45 hawapelekwi shule haswa kutokana na unyanyapaa na ubaguzi na kati ya wale wanaohudhuria shule asilimia 68 hawahudhurii kila siku na asilimia 37 tu humaliza elimu ya msingi.
Dk Njenje amesema watu wenye kifafa walio kwenye umri wa kuoa au kuolewa asilimia 67 hawajaoa au kuolewa na
Kati ya asilimia 33 waliooa au kuolewa wana viwango vikubwa zaidi vya talaka.
Hata hivyo amesema matokeo ya utafiti uliopo sasa yanaonesha kupungua kwa idadi ya waathirika wa kifafa kutoka zaidi ya 70 mpaka kati ya 20 na 15 kwa kila watu 1000.
Dk Njenje amesema pia waathirika wapya wamepungua kutoka zaidi ya 73 hadi karibia 50 kwa kila watu 100,000 kwa mwaka katika baadhi ya maeneo nchini kutokana na jitihada zilizofanywa na serikali.
“Kupungua huku kwa wastani ni kutokana na jitihada za pamoja za Wizara ya Afya kupitia programu ya Afya ya Jamii na mashirika ya kitaalamu yasiyo ya kiserikali kama chama chetu, mashirika yasiyo ya kiserikali na Wazazı wenye watoto wenye kifafa katika kukuza ufahamu na uelewa.
Aidha amesema kifafa ni ugonjwa wa kudumu wa ubongo unaoathiri takribani watu milioni 60 ulimwenguni kote huku ukiathiri watu 34 hadi 76 kwa kila wagonjwa 100,000 wapya wanaoongezeka kila mwaka.
“Tanzania ni mmoja ya nchi zenye baadhi ya vijiji vyenye idadi kubwa ya walioathirika hadi kufikia watu 37.5 kwa kila watu 1000 ikiwa na watu 73 hadi 111 kwa kila wagonjwa 100,000 wapya wanaoongezeka kila mwaka,”amesema.
Dk Njenje amesema kuwa msisitizo mkubwa zaidi unapaswa kuelekezwa kwenve mafunzo na usimamizi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa ajili ya kuzuia na utambuzi wa mapema wa kifafa.
Amesema Chama cha Wataalamu wa Kifafa, kimeanzisha mradi wa kituo cha mafunzo ya tiba saidizi/ujuzi huko Mahenge mkoani Iringa.
“Hapo baadaye tunahitaji vituo kama hivyo vilivyojikita kwenye mahitaji ya wale wenye ulemavu wa kimwili na katika kujifunza haswa watoto wenye kifafa na kwa sasa hatuna vituo rasmi vya tiba saidizi kwa watu wanaoishi na kifafa isipokuwa vituo vitatu vinavyoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali katika vituo vya Kanisa Katoliki,” amesema Dk Njenje.
Chanzo: Habari Leo