
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amekerwa na baadhi ya watoa huduma katika kituo cha huduma kwa wateja cha Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa kuwa wanasababisha malalamiko kwa wananchi.
Dk Biteko amesema hayo wakati wa kikao cha tatu cha tathmini ya uendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati katika kipindi cha Oktoba-Desemba 2024. Amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco kuchukua hatua kwa mtoa huduma aliyehusika na suala hilo na kutoa siku mbili.
Amesema Tanesco isipochukua hatua, yeye atafanya hivyo. Amesema anafahamu changamoto za watoa huduma hao
kupitia wananchi ambao wamekuwa wakimpa mrejesho.
“Mimi nafahamu changamoto za kituo hiki si kwa kuota bali wananchi wananipa mrejesho pamoja na viongozi wanaonisimamia,” alisema.
Dk Biteko alitoa mfano wa lalamiko la mwananchi aliyepiga simu Tanesco na kupewa namba ya tiketi ya lalamiko lake lakini baada ya muda, namba hiyo ikafutwa kwa madai kwamba lalamiko husika limeshashughulikiwa huku ikiwa si kweli na baada ya mteja kuuliza sababu ya kufutwa, aliishia kufokewa. Ameagiza watoa huduma hao wawe na heshima kwa wananchi na wataalamu.
Alisema kituo cha huduma kwa wateja wanapaswa kuwapa majibu stahiki na ya staha wananchi na wawe sehemu ya kutatua shida za wananchi.
“Pamoja na kazi zote nzuri mnazozifanya, lakini eneo ambalo bado hatujafanya vizuri ni utoaji wa huduma kwa wateja, juzi nilitembelea kituo hiki nikawaambia sifurahishwi na utendaji kazi wa kituo,” alisema.
Aliongeza: “Hivi tumefanya kazi yote hii ya kuwa na umeme wa ziada, tunajenga laini za umeme, lakini mtu mmoja ambaye kazi yake ni kumsikiliza mteja na kumpa majibu sahihi anatuchora wote vibaya tunaonekana hatufai, majibu yapo lakini wataalamu wanageuka kuwa wababe kwa wateja, hii haikubaliki.”
Dk Biteko ameziagiza taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Nishati kuupa kipaumbele Mpango wa Mahususi wa Nishati ambao ulisainiwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliofanyika Januari 27 na 28, 2025 ambao pamoja na masuala mengine ya nishati, umelenga kusambaza umeme kwa Watanzania milioni 8.3 ifikapo 2030.
“Kila mmoja kwa nafasi yake ajipange atatekeleza vipi hii Energy Compact (mpango wa mahususi wa nishati), fedha hizi mlizosikia zimetolewa na wadau wa maendeleo kama Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika zinahusu bara lote la Afrika, hazitakuja Tanzania pekee,” alisema.
Aliendelea, “…hivyo lazima tujipange jinsi ya kupata hizi fedha ili kutekeleza miradi tuliyopanga kuifanya na tumheshimishe Rais Samia kwa kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji mpango huu mahsusi ambao ni muhimu katika sekta yetu ya nishati.”
Wakati huo huo Dk Biteko amewaagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kazi ya usambazaji wa nishati safi ya kupikia vijijini inaenda sambamba na tathmini ya idadi ya watu wanaohama kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi kwenda kwenye nishati safi.
Ametaka ijipange kuhakikisha ifikapo 2030 asilimia 75 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Chanzo: Habari Leo