Anguko la Bilionea wa Congo Katika Mtego wa Madawa ya Kulevya. Eric Mandala Kinzenga, jina linalotetemesha miji mikubwa ya Afrika, alikuwa mfano wa ndoto ya kila Kiafrika. Tajiri huyu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), anayejulikana kwa utajiri wake wa kupindukia, alifahamika kwa maisha ya kifahari, magari ya kifahari, na sherehe za kifahari zilizovutia wakubwa kwa wadogo.
Lakini nyuma ya pazia la mafanikio hayo, kulikuwa na giza ambalo hatimaye limekuja kuonekana baada ya kukamatwa kwa tuhuma za madawa ya kulevya. Mandala ni bilionea wa kipekee. Kwa wengi, yeye alikuwa mfano wa kijana aliyepambana kutoka chini hadi kileleni. Utajiri wake ulitokana na biashara mbalimbali, ikiwa ni pamoja na madini, mafuta, na ujenzi, ambazo zilimpa heshima kubwa nchini Congo na kwingineko barani Afrika.
Hata hivyo, maisha ya Mandala yamejaa mambo ya kifahari kupitiliza. Kila mahali alipoenda, msafara wa magari ya kifahari kama Rolls-Royce, Lamborghini, na Ferrari ulikuwa ishara ya uwepo wake. Anamiliki majumba ya kifahari katika miji mikuu ya Afrika kama Kinshasa, Johannesburg, na Nairobi, pamoja na majumba mengine huko Paris na Dubai. Lakini mambo yamebadilika ghafla baada ya safari moja ya kibiashara kwenda Ulaya.
Mandala, ambaye mara nyingi anasafiri kwa ndege zake binafsi, alikamatwa akiwa na mzigo mkubwa wa madawa ya kulevya, tukio ambalo liliibua maswali mengi kuhusu chanzo halisi cha utajiri wake.
Alikamatwa akiwa na kilo 200 za cocaine zilizofichwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa kwenye maegesho ya kituo cha maduka. Shehena hiyo, inayotoka Ecuador na kupitia bandari ya Algeciras, ilipelekwa Morocco. Operesheni hiyo iliyofanywa na DEA na Udyco, inafuatia uchunguzi uliodumu kwa miezi kadhaa uliozinduliwa Agosti 2024.
Mandala, ambaye tayari alikuwa chini ya uangalizi, alikamatwa akiwa na mwanamke wa Colombia, akiwa na zaidi ya dola 50,000 taslimu.
Ripoti zinasema kwamba Mandala alikuwa akitumia biashara zake halali kama kisingizio cha kufanikisha usafirishaji wa madawa ya kulevya kutoka Amerika Kusini hadi Ulaya, huku akitumia Congo kama kitovu cha operesheni zake. Polisi walipata ushahidi wa meli na ndege binafsi zilizokuwa zikitumiwa kusafirisha shehena kubwa za madawa hayo. Baada ya kukamatwa kwake, uchunguzi ulianza kufuatilia mtandao wa Mandala.
Ripoti zimefichua kwamba bilionea huyu alikuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya Congo, na kwamba amekuwa akitumia mali yake kununua ushawishi na kufanikisha mipango yake haramu. Mandala pia anahusishwa na vikundi vya kihalifu vilivyoenea Afrika Magharibi na Amerika Kusini.
Inasemekana kuwa amefanya mikataba na magenge makubwa ya Mexico na Colombia, akiwasaidia kusafirisha madawa yao kwa usalama kupitia njia zake za kimataifa. Watu wengi nchini Congo wamegawanyika kuhusu habari hii. Wapo wanaomuona Mandala kama shujaa wa taifa ambaye alileta ajira na maendeleo, lakini wengine waliona utajiri wake kama matokeo ya uhalifu uliochangia kuharibu jamii.
Mwandishi mmoja wa habari wa Kinshasa alisema. “Mandala alikuwa akionekana kama shujaa wa watu maskini, lakini sasa tunaona upande wake wa giza. Madawa ya kulevya si tatizo la Ulaya tu, ni janga ambalo limeathiri hata vijana wetu hapa Congo.”
Kwa mujibu wa ripoti, Mandala amekanusha mashtaka yote, akidai kuwa alikuwa amewekewa mtego na mahasimu wake wa kibiashara. Lakini ushahidi wa mawasiliano yake na magenge ya kimataifa, pamoja na mali zilizokuwa zikihusishwa moja kwa moja na biashara ya madawa, umekuwa mzito mno kupuuzwa.
Kama atapatikana na hatia, Mandala anakabiliwa na kifungo cha maisha gerezani, jambo ambalo litaleta anguko kubwa kwa mtu ambaye aliwahi kuchukuliwa kama mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa barani Afrika.
Je, alikuwa ni bilionea aliyepata utajiri wake kwa njia halali, au ni mfano mwingine wa jinsi madawa ya kulevya yamepenya kwenye mifumo ya kiuchumi barani Afrika?

Pichani ni KITABU Cha bwana Eric Mandala ambacho anahamasisha Jamii juu ya utafutaji na uvumilivu. Hapo ndio tutagundua kuwa kumbe mwendo aendao Kila tajiri sio wa kuuiga.