Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, ametekeleza ahadi yake kwa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita (GPC) kwa kukabidhi pikipiki tatu zitakazorahisisha kazi za uandishi wa habari katika mkoa huo.
Katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika leo, Mheshimiwa Kanyasu amepongeza juhudi za waandishi wa habari katika kuhabarisha na kuelimisha jamii, akisema kuwa mchango wao ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.
“Ninatambua kazi kubwa inayofanywa na waandishi wa habari katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati. Pikipiki hizi zitawasaidia kuwafikia wananchi kwa haraka na kufanya kazi yenu kwa ufanisi zaidi,” alisema Mheshimiwa Kanyasu.
Mwenyekiti wa GPC, Bw. Renatus Masuguliko, amepongeza juhudi za Mbunge huyo na kueleza kuwa msaada huo utakuwa chachu ya kuboresha mazingira ya kazi kwa wanahabari wa Geita.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Kanyasu kwa kutimiza ahadi yake. Pikipiki hizi zitatuwezesha kufuatilia matukio kwa wakati na kuhakikisha habari zinawafikia wananchi haraka,” alisema Bw. Masuguliko.
Hafla hiyo imehudhuriwa na waandishi wa habari wa Geita pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya habari, ambao wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana katika kuboresha mazingira ya kazi kwa wanahabari nchini.


