Kama mnavyokumbuka kwamba, Jeshi la Polisi Mkoani Geita Februari 21, 2025 lilitoa taarifa kwa umma kuhusiana na kuwashikilia wanafunzi thelathini (30) wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya Geita iliyopo Manispaa ya Geita kutokana na vitendo vya kufanya vurugu shuleni hapo Februari 20, 2025 majira ya saa 2 usiku.
Jeshi la Polisi limekamilisha uchunguzi wa tukio hilo kwa kuwahoji wanafunzi thelathini (30) waliokamatwa Februari 20, 2025 na wengine 41 na kufanya wanafunzi waliohojiwa kuwa sabini na moja (71). Uchunguzi wa tukio hilo umekamilishwa kwa kushirikiana na Bodi ya Shule ya Sekondari ya Geita na tayari hatua zimechukuliwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za shule dhidi ya wanafunzi sabini na moja (71) waliobainika kuhusika kwenye tukio hilo.
Wanafunzi saba (07) wamefukuzwa Shule ambao ni Laban Manjano aliyelikuwa kiranja mkuu wa Shule hiyo mwaka 2024 alihamasisha mgomo na vurugu hizo, Elias Zacharia, Harrizon Malinga, Ahmed Mashaka, Frank Paulo, Erick Atanga na Alphonce Makelemo.
Aidha, waliosimamishwa shule hadi Mei 05, 2025 ni Wanafunzi 19 na wanafunzi 45 wamesimamishwa shule kwa muda wa siku 21.