Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watu watatu wa familia moja kwa tuhuma ya Mauaji ya baba yao mzazi aitwaye Hussein Bundala, mwenye umri wa miaka 103 aliyeuawa akiwa nyumbani kwake Februari 05, 2025 majira ya saa 2 usiku katika Kitongoji cha Ihananilo, Kata ya Nyamtukuza Wilaya ya Nyang’hwale kwa kukatwa na kitu chenye makali sehemu za kichwani, usoni na shingoni.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Yombo Hussein Bundala, Mwanamke, Miaka 75; Makame Hussein Bundala, Mwanaume, Miaka 53 na Shija Hussein Bundala, Mwanaume, Miaka 50.
Jeshi la Polisi linakamilisha uchunguzi wa tukio hili kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kiuchunguzi na watuhumiwa watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Jeshi la Polisi linalaani vikali vitendo hivi na litahakikisha kila anayeshiriki katika vitendo vya kihalifu anakamatwa na kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.