Jeshi la Polisi linathibitisha ajali iliyotokea Februari 24, 2025 saa 2 usiku katika eneo la Mpomvu, Kata ya Mtakuja, Wilaya ya Geita ambapo Basi aina ya TATA lenye namba za usajili T.422 DMQ mali ya kampuni ya SOMA lililokuwa likitokea Geita Mjini kwenda Katoro likiendeshwa na dereva aitwaye Hakimu Changa, umri 39, Mnyakyusa liligonga Pikipiki SANLG yenye namba za usajili MC.730 CLS na kusababisha vifo, majeraha na uharibifu wa mali.
Waliofariki katika ajali hiyo ni dereva wa pikipiki tajwa pamoja na abiria mmoja ambao wote hawajatambulika na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa taratibu za uchunguzi na utambuzi. Aidha, mtu mmoja ambaye alikuwa abiria wa pili kwenye pikipiki hiyo amepata majeraha makubwa kichwani na kuvunjika miguu yote miwili, anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Geita.
Imebainika, chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa Basi kushindwa kuwajali watumiaji wengine wa barabara. Dereva wa Basi tajwa aitwaye Hakimu Changa, umri 39, Mnyakyusa mkazi wa Mwanza amekamatwa kwa mahojiano. Uchunguzi wa ajali hii unakamilishwa kwa haraka na upo katika hatua za mwisho na mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani muda wowote kuanzia sasa.