Serikali katika wilaya ya chato Mkoani Geita imewaomba wadau wa elimu kuendelea kushirikiana na serikali ili kutatua upungufu wa madawati kwa wanafunzi wa shule za Msingi na sekondari wilayani humo.
Rai hiyo imetolewa na katibu tawala wilaya ya Chato Thomas Dime wakati akimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo katika hafla ya kukabidhi madawati, viti pamoja na vifaa tiba kwenye shule ya Msingi Mkuyuni vilivyotolewa na benki ya Nmb katika wilaya hiyo vilivyotolewa kwa lengo la kutatua changamoto katika sekta ya elimu pamoja na afya.
Dime amesema wilaya ya Chato inakabiliwa na upungufu wa madawati zaidi ya elfu 26 kwa shule za Msingi pamoja na elfu 6 kwa shule za sekondari na kuwaomba wadau wa elimu, serikali kupitia Halmashauri pamoja na wananchi kushirikiana kutatua tatizo hilo.
Meneja wa benki ya Nmb kanda ya ziwa Faraja Raphael Ng’ingo amevitaja vifaa hivyo vilivyotolewa na benki hiyo vimegharimu kiasi cha shilingi Milioni 29.5 na vitainufaisha hospitali ya Rufaa kanda ya Chato, shule ya Rubambagwe, Itale, Lumasi pamoja na shule ya Msingi Mkuyuni.
Mbunge wa jimbo la Chato Dk. Medard Matogoro Kalemani na Mwenyekiti wa kijiji cha Mkuyuni cha Mkuyuni Goodluck Phinias wameishukuru benki ya Nmb kwa msaada wake na kuomba kuendelea kujitoa katika kuchochea maendeleo ya wilaya ya Chato katika nyanja mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Serikali Wilaya ya Chato kupitia kwa katibu tawala wa wilaya hiyo Thomas Dime inaeleza kuwa wilaya hiyo kwa kushirikiana na wakala wa misitu TFS wamepanga kutumia misitu iliyopo kutengeneza viti na meza kukabiliana na tatizo hilo .





