Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini wametakiwa kuanzisha kliniki ndogondogo za walimu ili kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili.
Rai hiyo imetolewa, Februari 26, 2025, na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Mashaka Biteko, wakati wa kliniki ya kusikiliza na kutatua kero za Walimu iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu, Manispaa ya Geita.
Dkt. Biteko amesema kuwa baadhi ya changamoto za walimu zinaweza kutatuliwa katika ngazi za halmashauri bila kufikishwa kwenye ngazi za juu za serikali, endapo tu walimu watawasilisha kero zao kwa wakati kupitia viongozi wao wa halmashauri.
Akizungumzia mafanikio ya sekta ya elimu katika serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Biteko amesema kuwa zaidi ya walimu 10,839 wamepandishwa madaraja, huku shilingi bilioni 4.6 zikitumika kuwalipa madeni na malimbikizo ya mishahara walimu 5,061. Aidha, walimu 876 wamebadilishiwa muundo wa ajira baada ya kujiendeleza kielimu.
Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita inatambua na kuthamini mchango wa walimu katika maendeleo ya sekta ya elimu, ambapo shilingi milioni 25 zimetumika kwa ajili ya matibabu ya walimu katika Mkoa wa Geita kwa mwaka 2024.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Paschal Katambi, amesema serikali imefanya mabadiliko katika sera na sheria za utumishi wa umma, ikiwemo sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii PSSF na NSSF, ili kuendana na mahitaji ya sasa na kuondoa kero zinazowakabili watumishi, wakiwemo walimu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela, amepongeza Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kubuni mbinu bora za kutatua kero za walimu kwa kuwakutanisha na serikali.
Kliniki hiyo imeratibiwa na CWT kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Wizara ya Fedha, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC-HQ).