Chato, Geita – Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, amesema sauti ya wanawake ni sauti ya Mungu na wengi, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Kalemani alitoa kauli hiyo Machi 1, 2025, wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Wanawake na Samia katika Kata ya Bwanga, Wilaya ya Chato, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi yenye utulivu, amani, na mshikamano mkubwa, hali ambayo imechochewa na uongozi wa Rais Samia.
Alieleza kuwa serikali imewekeza katika maendeleo ya miundombinu mkoani Geita, hususan katika Kata ya Bwanga, ambapo huduma za umeme, maji safi, barabara za lami, na stendi ya mabasi zipo katika hali nzuri.
Mbunge huyo aliwataka wanawake kupitia taasisi hiyo kushiriki kikamilifu katika kueneza mafanikio ya Rais Samia kwa Watanzania wote. “Sauti ya wanawake ni sauti ya Mungu na ya wengi, hivyo ni muhimu kuzungumza mazuri yanayofanywa na serikali,” alisisitiza Dkt. Kalemani.