Watu sita wamefariki dunia na wengine 49 wamejeruhiwa baada ya kutokea ajali katika eneo la Chigongwe Jijini Dodoma majira ya saa 4 usiku wa Machi 03,:2025.
Ajali hiyo imehusisha lori na basi lenye namba za usajili T405 BYS, mali ya kampuni ya AN Classic lililokuwa likitokea Dodoma kuelekea Kigoma.
Mashuhuda wa ajali hiyo wamedai kuwa lori lililohusika katika ajali hiyo lilikuwa limeharibika barabarani na hakukuwekwa alama yoyote ya tahadhari, na hivyo kuchangia kutokea kwa ajali hiyo.
Wengine wamedai kuwa mwendokasi wa basi hilo unaweza kuwa chanzo cha ajali hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule akiwa na vyombo vya usalama alifika katika eneo la ajali na kusema kuwa majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kupatiwa matibabu, huku 23 kati yao ikielezwa tayari wamefanyiwa upasuaji.
Miili ya watu waliofariki dunia katika ajali hiyo nayo imehifadhiwa katika hospitali hiyo, kusubiri utambuzi wa ndugu zao.