WAKAZI wa Dar es Salaam wameanza kujiandikisha na wengine kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mchakato huo ulianza Jumatatu huku Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikihimiza wananchi waendelee kujitokeza.
Tunaipongeza serikali kupitia INEC kwa uratibu na usimamizi thabiti wa mchakato huu ambao umeshakamilika katika mikoa 29 na sasa ipo kwenye mzunguko wa mwisho Dar es Salaam pekee.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele, sasa wapo katika mzunguko wa 13.
Mchakato huu, ulioanza Dar es Salaam Jumatatu, ukitarajiwa kukamilika Machi 23, 2025 ni sehemu muhimu ya demokrasia nchini ukitoa fursa muhimu kwa kila Mtanzania kuhakikisha kuwa anajiweka sawa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Uandikishaji au uboreshaji wa daftari hili ni jukumu muhimu kwa kila mwananchi anayekidhi vigezo kushiriki.
Hivyo, hatuna budi kuungana na INEC kuhimiza wakazi wa Dar es Salaam kutumia siku hizo zilizopangwa kukamilisha kazi hiyo.
Hata hivyo, kumekuwapo na utamaduni uliojengeka katika jamii, ambapo baadhi ya watu hujisahau kushiriki masuala kama haya siku za mwanzoni badala yake husubiri hadi siku za mwishoni.
Huu ni utamaduni mbaya ambao jamii haina budi kuondokana nao hususani kipindi hiki cha uandikishaji Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kwa wananchi wasio na sababu muhimu za kusubiri, wawahi wakajiandikishe ili kuepusha misururu isiyo ya lazima katika siku za mwishoni. Hali hiyo mara nyingi husababisha malalamiko mengi kuhusu huduma.
Tunapenda kuwahimiza wakazi wote wa Dar es Salaam kujitokeza mapema ili kushiriki katika mchakato huu wenye manufaa makubwa kwa taifa na watu wake.
Kuboresha au kujiandikisha katika daftari hilo la mpigakura ni haki ya kila Mtanzania anayekidhi vigezo ajitokeze
katika vituo vilivyopangwa aipate.
Izingatiwe kwamba serikali imetenga rasilimali nyingi kwa ajili ya mchakato huu. Kwa hiyo, ni wajibu wa kila mwananchi kuunga mkono mchakato huu wa kidemokrasia.
Rai yetu kwa wakazi wa Dar es Salaam ni kwamba wahimizane kujiandikisha mapema ili kuepuka msongamano
baadaye. Hii ni fursa adhimu.
Mchakato huu uchukuliwe kwa uzito ili matarajio ya INEC yatimie; ya kuandikisha wapigakura wapya 643,420 mkoani Dar es Salaam ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya 3,427,917 waliopo kwenye daftari la kudumu la wapigakura.