Mnamo mwaka wa 2006, sekta ya vinywaji baridi ilikumbwa na kashfa kubwa ya ujasusi wa kibiashara baada ya mfanyakazi wa Coca-Cola kujaribu kuuza siri za kampuni hiyo kwa mshindani wake mkuu, PepsiCo, kwa dola milioni 1.5. Katika hali ya kushangaza, Pepsi haikukubali ofa hiyo na badala yake ilichukua hatua ya kiungwana kwa kuarifu Coca-Cola kuhusu mpango huo.
Kwa mujibu wa ripoti, Joya Williams, aliyekuwa msaidizi wa kiutawala katika makao makuu ya Coca-Cola huko Atlanta, alikuwa mhusika mkuu katika njama hiyo. Williams alishirikiana na washirika wake wawili, Ibrahim Dimson na Edmund Duhaney, ambapo walipanga kuiba nyaraka za siri na sampuli za kinywaji kipya cha Coca-Cola na kuuza kwa mshindani wao mkubwa, Pepsi.
Kila kitu kilianza pale mtu aliyejitambulisha kwa jina la bandia “Dirk” alipowasiliana na Pepsi akidai kuwa na taarifa za siri za Coca-Cola. Badala ya kutumia fursa hiyo kwa manufaa yao, Pepsi walichukua msimamo wa kimaadili na kuarifu Coca-Cola kuhusu njama hiyo. Coca-Cola ilihusisha Ofisi ya Upelelezi ya Marekani (FBI), ambayo ilianzisha uchunguzi wa siri ili kuwatega wahusika.
Mnamo Juni 2006, FBI ilifanikiwa kupanga mtego wa kuwanasa washukiwa. Katika mkutano wa kwanza kati ya wakala wa FBI na “Dirk,” Dimson alikabidhi nyaraka za siri na sampuli ya kinywaji kwa malipo ya awali ya dola 30,000.
Baada ya kuthibitisha uhalali wa taarifa hizo, wakala alikubaliana kukutana tena kwa malipo makubwa zaidi ya dola milioni 1.5. Katika mkutano huo wa pili, watatu hao walikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya ujasusi wa kibiashara na wizi wa siri za kampuni.
Pepsi ilitoa taarifa ikisema, “Tulifanya kile ambacho kampuni yoyote inayowajibika ingefanya. Ushindani unaweza kuwa mkali, lakini lazima uwe wa haki na wa kisheria.” Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Coca-Cola, Neville Isdell, aliwashukuru Pepsi kwa uadilifu wao na kuhimiza wafanyakazi wa Coca-Cola kuwa waaminifu na kulinda siri za kampuni.
Tukio hili liliibua mjadala mpana kuhusu ujasusi wa kibiashara na maadili ya ushindani wa kibiashara. Licha ya ushindani mkali kati ya Coca-Cola na Pepsi, hatua ya Pepsi ya kuarifu mamlaka ilionyesha mfano wa uaminifu na maadili katika sekta ya biashara.
Je, unadhani ingekuwa huku kwetu Tanzania mambo yangekuwaje?