Kampuni ya mabasi yaendayo haraka (UDART) inajiandaa kupokea mabasi mapya yanayotumia gesi asilia iliyosindikwa (CNG) kuanzia mwezi Aprili 2025.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma za usafiri jijini Dar es Salaam kwa kutumia nishati safi na nafuu. Ujio wa Mabasi hayo mapya unalenga kupunguza msongamano wa abiria na kuchangia katika uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya mafuta ya dizeli.
Hatua hiyo ya kuingiza mabasi mapya inalenga kuyaondoa kwa awamu mabasi machakavu na yale ambayo muda wake wa kuwa barabarani yamepitwa na wakati likiwemo basi moja ambalo hivi karibuni limeonekana kwenye mitandao ya kijamii likipitisha maji sehemu yake ya kupitishia hewa (ventilation).
“Tunatarajia mabasi haya yatasaidia kuongeza ufanisi wa huduma zetu na kupunguza muda wa kusubiri kwa abiria,” Amesema msemaji wa UDART Gabriel Katanga
Mabasi yanayotumia gesi asilia (CNG) yanajulikana kwa kuwa rafiki wa mazingira, kwani hutoa kiwango kidogo cha hewa chafu ikilinganishwa na mabasi ya dizeli.
UDART imesisitiza kuwa mpango huu ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani katika kuboresha huduma za usafiri wa umma na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hatua hiyo ya kuagizwa kwa mabasi mapya katika huduma za usafiri wa mabasi yaendayo haraka inatekelezwa kufuatia kuwepo kwa changamoto ya mabasi ya awali yaliyohudumu kwa muda mrefu na kupelekea uchakavu ambapo muda wa matazamio ya kihuduma katika mabasi hayo kulingana na taarifa za mzalishaji wa Mabasi hayo ni miaka 8 hadi 10. Mabasi ya awali yaliingizwa nchini mara ya kwanza kati ya mwaka 2015-2016.
Kampuni ya Mabasi yaendayo haraka (UDART) imeeleza kuwa ujio wa mabasi mapya ni hatua muhimu kuelekea kupunguza msongamano wa abiria na kuboresha huduma kwa ujumla.
“Tunataka kuhakikisha kuwa teknolojia ya mabasi yanayotumia gesi asilia inakidhi mahitaji ya wakazi wa Dar es Salaam kabla ya kuanza operesheni rasmi za mabasi mapya mwaka huu” Kauli toka kwa Msemaji wa UDART Gabriel Katanga