Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limekanusha madai kuwa gari lake lilitumika kubeba wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mnamo Machi 22, 2025, kama ilivyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo, gari la polisi lenye namba PT.4342 lilikuwa likitoka Wilaya ya Itilima kuelekea Bariadi kwa kazi maalum. Katika Kijiji cha Budalabujiga, askari walilikuta gari jingine lenye namba T.356 AAK, mali ya Kampuni ya Allince, likiwa limeharibika.
Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Itilima, aliyekuwa kwenye gari hilo la polisi, aliamuru kusimamisha ili kufahamu hali ya abiria waliokuwa kwenye gari lililoharibika. Wananchi waliokuwa kwenye gari hilo walieleza kuwa walikuwa wakisafiri kuelekea Bariadi na waliomba msaada wa usafiri kutokana na hali mbaya ya hewa iliyosababishwa na mvua
Kutokana na hali hiyo, na kwa kuzingatia wajibu wa Jeshi la Polisi wa kulinda usalama wa raia na mali zao, Mkuu wa Upelelezi aliruhusu wananchi hao kupanda gari la polisi na kuwafikisha Bariadi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limeeleza kuwa kitendo hicho kilikuwa ni msaada wa kibinadamu na si kubeba wanachama wa chama chochote cha siasa kama inavyodaiwa kwenye mitandao ya kijamii. Polisi wamewataka wananchi kuzingatia ukweli na kuepuka kusambaza taarifa zisizo sahihi zinazoweza kuchochea taharuki.
