Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameviagiza vyombo vya usalama barabarani nchini kuongeza nguvu katika usimamizi wa sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni madereva wote wanaosababisha ajali za barabarani zinazopelekea vifo, ili kupunguza na hatimaye kutokomeza kabisa wimbi la ajali nchini.
Dkt. Samia ametoa agizo hilo wakati akitoa salamu za pole kufuatia tukio la ajali ya barabarani liyotokea Aprili 3, 2025 na kuhusisha basi la abiria mali ya kampuni ya Mvungi, lililokuwa likitoka Ugweno wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, kuelekea Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilipelekea vifo vya watu nane huku wengine 41 wakijeruhiwa ambapo inaelezwa kwamba ilitokana na basi hilo kuacha njia ilipokuwa inapishana na gari ndogo na hatimaye kuserereka kwenye mlima katika eneo la Kikweni, kata ya Msangeni wilayani humo.
Mbali ya maelekezo hayo kwa vyombo vinavyohusika na usimamizi wa usalama barabarani nchini, Dkt. Samia pia amewataka watumiaji wote wa barabara kuhakikisha wanakuwa waangalifu na kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza majanga ya ajali yanayosababisha vifo na majeruhi wengi kila mwaka.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi kuhusu agizo hilo la Dkt. Samia, Irene Msellem ambaye ni balozi wa usalama barabarani kupitia shirika la RSA Tanzania amesema
“Ni hatua ambayo itasaidia sana ikiwa itatekelezwa na wasimamizi wa sheria, sote tunafahamu kwamba ajali nyingi zinatokana na uzembe wa watumia barabara hususan madereva ambao makosa mengi wanayofanya yanayo sababisha ajali ni yenye kujirudia rudia, hii ikimaanisha adhabu za faini haziwafanyi wajutie na kujifunza hivyo hili la kufungiwa leseni linaweza kusaidia wakabadilika haraka zaidi”
Aidha, balozi Irene amewaomba Watanzania kufahamu kwamba ajali nyingi zinaweza kuepukika ikiwa watumia barabara hususan abiria kwenye vyombo vya moto watatimiza wajibu wao mkubwa ambao ni kuelimisha, kukemea na kuripoti matukio yote ya barabarani wanayoona yanafanywa na madereva yakihatarisha usalama wao au wa watumiaji wengine wa barabara
