Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima ametoa taarifa inayothibitisha kupokea videos zinazoonesha mabinti kadhaa wakishirikiana kumdhalilisha binti mwingine kwa maneno na vipigo na mambo mengine mabaya ambapo, watoa taarifa waanadai kuwa mabinti hao wote ni wanafunzi wa vyuo vikuu viwili tofauti nchini huku wengine wakidaiwa kuwa, wanasoma darasa moja na huyo binti wanayemdhalilisha na kumrekodi.
Aidha, kwenye mazungumzo yao kama yanavyosikika, inaonekana ni ugomvi wa kumgombania mwanaume anayetajwa kwa jina moja la Mwijaku.
Waziri Gwajima aameonyesha kusikitishwa kusikia mabinti aliowaita wasomi ambao, wangetakiwa kujikita kwenye elimu na kuunganisha nguvu kupambana kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto badala yake wanatumia nguvu zao na elimu zao kukatiliana, kudhalilishana na kujidhalilisha wao kwa wao.
Hivyo ameweka wazi kuwa amechukua hatua kwa kuwasiliana na muhanga wa tukio hilo na kumuunganisha na huduma za ustawi wa jamii, msaada wa kisaikolojia na huduma za dawati la jinsia Polisi ambapo pia atapata msaada wa kisheria ili haki itendeke pia, amebainisha kuwa anawasiliana na wakuu wa vyuo ili haki itendeke pamoja na Waziri wa Elimu kwa hatua zaidi.