Mbio za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 zinazidi kushika kasi. Ni uchaguzi ambao Watanzania watamchagua rais wa Jamhuri ya Muugano, wabunge, madiwani na upande wa Zanzibar, watachagua rais, wawakilishi na nafasi sawa na za Tanzania bara.
Huu ni uchaguzi wa saba tangu kurudi kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Lakini ndio wa kwanza kwa chama tawala CCM, kuweka mgombea mwanamke, ambaye anatarajiwa kuwa rais wa sasa Samia Suluhu Hassan.
Tangu Bunge la 12 la Tanzania kukamilisha rasmi shughuli zake tarehe 27 Juni 2025. Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kumesheheni picha za watia nia hasa katika nafasi ya Ubunge – na watia nia wengi wanaonekana kuelekea chama tawala.
Watia nia wako makundi mawili; wale ambao wamezoeleka kuonekana katika shughuli za kila siku za Chama cha Mapinduzi (CCM), na hakuna anayefumbua mdomo akisikia wanataka kugombea ubunge. Kundi la pili, ni watia nia ambao hawana kabisa historia ya kujishughulisha na shughuli za wazi za CCM.
Kwanza ieleweke kwamba kuchukua fomu ya kugombea uongozi wa kisiasa ni haki ya kila anayekidhi vigezo, kupitia chama chochote kile atakacho. Lakini hilo, linakwenda sanjari na ukweli kwamba kuzijadili siasa vilevile ni haki ya kila mtu.
Takwimu zinasemaje?
Kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, wanachama 5,475 wamechukua fomu kuwania nafasi za Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.
Baada ya kufungwa kwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu ndani ya CCM, kwa nafasi ya ubunge katika majimbo yote 272 ya uchaguzi nchini: Watia nia kutoka Tanzania Bara wapo 3,585. Watia nia kutoka Zanzibar ni 524. Kwa upande wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, jumla ya wagombea 503 wamechukua fomu. Kwa ujumla wagombea wa ngazi zote wakiwemo udiwani, wanafikia 20,000.
Makalla ameeleza, idadi hiyo inaonesha mwitikio mkubwa wa wanachama wa CCM katika kushiriki kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama, na hatua inayofuata ni mchakato wa uchujaji.
Kwa nini wanakimbilia CCM?
Jawabu ya swali hili, litategemea unamuuliza nani. Bila shaka CCM itasema ni dalili ya kukubalika kwao. Chama ni kikongwe na kimejipanga. Hoja hiyo itatiliwa mkazo na ushawishi ambao bado chama hicho kinao ndani ya siasa za Tanzania.
Ingawa wapinzani wao wanaweza kujenga hoja kuwa, wengine wanakimbilia CCM kwa sababu ya kutegemea mteremko. Hoja hii itatiliwa mkazo na kile kilichotokea katika uchaguzi wa 2020. CCM ilipopata ushindi mkubwa wenye utata katika ngazi zote za udiwani, ubunge na uwakilishi. Ingawa CCM wenyewe pamoja na Tume ya Uchaguzi wakati huo (NEC) ilisisitiza uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Mbali na jawabu hizo, kuna jawabu la tatu la swali hili. Nilipomuliza mchambuzi wa siasa za Tanzania, Thomas Kibwana, kwa nini kuna idadi kubwa ya watia nia wanaokimbilia CCM?
“Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakijasaini fomu za maadili kwa ajili ya kushiriki uchaguzi mkuu mpaka sasa, kwa hiyo huenda wapo baadhi ya watu ambao labda wangegombea kupita Chadema, lakini wameamua kutafuta vyama vingine. Wengine tumewaona wakienda Chaumma na ACT Wazalendo, na wengine ndio hao wanakwenda CCM.”
Chanzo: BBC Swahili