Mvulana huyu mwenye miaka 13 alikamatwa akiiba Mkate dukani ambako wakati akimkimbia alipamia kona ya kabati nalo likavunjika.
Jaji aliyesikiliza shauri hili la Jinai akamuuliza Mtoto huyu kama kweli aliiba mkate na kujaribu kukimbia, Mtoto akasema ndio. Alipoulizwa kwa nini akasema aliiba mkate huo kwakuwa aliuhitaji sana! Alipoulizwa kwanini hakuununua, akajibu hakuwa na fedha na kwamba nyumbani kwao, anaishi na mama yake pekee ambaye ni mgonjwa sana na hana kazi.
Kijana huyo aliendelea kusema;
“Mimi ninafanya kazi ya kuosha magari lakini nilishindwa kwenda kutokana na hali mbaya ya mama yangu, nikajulishwa kuwa nimefukuzwa kazi”
Jaji aliyekuwa akimsikiliza kijana huyo kwa makini akamuuliza kama alifanya jitihada nyingine zozote za kuhakikisha anapata fedha, ambapo kijana huyo alimueleza Jaji kwamba aliwaomba wapita njia zaidi ya 50, hakuna aliyemsaidia ndio akaona achukue hatua hiyo ili kumuokoa mama yake na njaa licha ya kujua kwamba alichokuwa anafanya ni kosa.
Akitoa hukumu yake Jaji aliyekuwa akisikiliza shauri hilo aliwashangaza waliohudhuria kusikiliza shauri hilo kutokana na maamuzi aliyoweza kuyafanya. Jaji huyo akisoma hukumu yake alisema;
“Wizi na hasa wizi wa mkate kwa mtoto mwenye njaa ni aibu na sisi sote (tulioko katika chumba hiki cha mahakama) tunahusika na jinai hii. Kila mmoja humu Mahakamani pamoja na mimi kama sehemu ya jamii iliyoshindwa kumsaidia mtoto mwenye njaa anayo hatia na ninamhukumu (kila mmoja aliye ndani ya chumba hiki) kulipa faini ya dola kumi na hakuna yeyote atakayetoka humu ndani bila kulipa.
Aliposema hayo akatoa pochi yake na kutoa dola kumi na kuiweka mezani kisha akaanza kuorodhesha majina ya wanaolipa.
Baada ya kumalizana na wasikiliza kesi waliokuwa ndani ya mahakama kwa wakati huo, Jaji akaendelea na hukumu yake kwa kusema;
“Naliadhibu pia duka lililoshindwa kumsaidia mtoto mwenye njaa, kulipa Dola 1000 kwa kumkamata mtoto mwenye njaa na kumkabidhi kwa Polisi. Kama duka hilo lisipolipa faini hii ndani ya saa 24 ninaamuru duka hilo lifungwe. Polisi nao watalazimika kulipa Dola 1000 kwa kumkamata Mtoto mwenye njaa na kumfungulia mashitaka kumleta hapa Mahakamani” alimaliza kusoma hukumu yake
Jaji baada ya kukusanya fedha zote za faini alipiga magoti na kumkabidhi mtoto yule na kumuomba radhi kwa niaba ya jamii iliyoshindwa kumsaidia yeye na mama yake mgonjwa.