Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imesema kwamba katika msimu huu wa mvua za masika, kunatarajiwa ongezeko la mvua katika mwezi wa Nne mwaka huu 2025.
Akizungumza na Torchmedia ofisini kwake jijini Dar es Salaam, mchambuzi wa hali ya hewa kutoka TMA, Joyce Makwata, amesema kwamba kulingana na mifumo ya hali ya hewa, inaonyesha uwepo wa ongezeko la mvua katika mwezi wa Nne katika kipindi hiki cha mvua za masika.
Aidha, amewasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa kila siku, ikiwemo kuchukua tahadhari mbalimbali ili kuepukana na athari za mvua zinazoweza kujitokeza.
Akizungumzia kuhusu uwepo wa joto, Makwata amesema kwamba joto litaendelea kupungua kulingana na mvua zinavyoendelea kunyesha.
Amesema kwamba uwepo wa mvua umeshusha joto kwa mkoa wa Dar es Salaam na nchi nzima kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Makwata amesema kuwa katika maeneo mengi nchini ambayo yako karibu na misitu au miti mingi, yanatarajiwa kupata mvua nyingi ukilinganisha na maeneo mengine.
Kwa Dar es Salaam, pia Hali Iko hivyo hivyo kwa maeneo ambayo yana misitu na miti ya yanatarajiwa kupata mvua za kutosha.
Msimu wa mvua za masika ni kipindi cha mvua zinazonyesha katika maeneo mbalimbali ya tropiki, hasa katika nchi za Afrika Mashariki, zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, na nchi zingine za ukanda huo. Mvua hizi hutokea kila mwaka, kwa kawaida, kuanzia mwezi Machi hadi Mei, ingawa kipindi hiki kinaweza kutofautiana kidogo kulingana na eneo na mwaka.
Mvua za masika ni muhimu kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara, kwani hupatia udongo unyevu unaohitajika kwa mazao kama vile mahindi, mpunga, na maharage. Hata hivyo, mvua hizi pia zinaweza kuleta changamoto, kama vile mafuriko, uharibifu wa miundombinu, na athari nyingine za kimaumbile.