Kikosi cha Simba Sports Club kilichotinga hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF Confederation Cup, kinatarajiwa kuondoka nchini alfajiri ya tarehe 28 kuelekea Misri kwa mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Al Masry.
Kwa mujibu wa msemaji wa klabu hiyo Ahmed Ally, kikosi chao kitaondoka kwa kutumia ndege ya Egypt Air ambapo wachezaji waliokuwa na Taifa Stars wataungana na timu nchini Misri. hata hivyo, mlinda mlango wao namba moja Mousa Camara na mshambuliaji Steve Desse Mukwala tayari wameshawasili nchini kujiunga na wachezaji wenzao kwa ajili ya maandalizi ya safari.”
“Kila Mwanasimba atambue kwamba pamoja na mipango tuliyonayo lakini lazima tujipange, lazima tujiandae na hasa kama timu yenyewe inatokea Misri. Ukiangalia michuano ya Afrika ilivyo utaona kwamba Misri ndio nchi iliyoingiza timu nne kwenye robo fainali, tunakwenda kucheza na Al Masry tukijua tunakwenda kucheza mechi ngumu kwelikweli lakini dhamira tuliyojiwekea ni kufuzu nusu fainali.” amesema Ahmed.
Kuhusu mechi ya marudiano ambayo itapigwa Tanzania, Ahmed amesema upo uwezekano mkubwa kwa mechi hiyo kupigwa kwenye dimba lao Uwanja wa Mkapa, baada ya kufanyiwa maboresho na wanaamini taarifa ya ukaguzi itakuwa nzuri.
“Niwatoe hofu kwamba Uwanja wa Benjamin Mkapa umeshafanyiwa ukaguzi. Bado majibu hayajatoka lakini katika mazungumzo wanasema kuna maboresho makubwa kwenye uwanja ukilinganisha na mara ya mwisho walipofanya ukaguzi hivyo kuna nafasi kubwa ya kucheza kwenye uwanja huo.”-
Kwa upande mwingine, Ahmed ametangaza kaulimbiu ya mchezo huo wa marudiano akisema
“Kaulimbiu ya mchezo dhidi la Al Masry itakuwa ni HII TUNAVUKA. Hii inamaanisha kwamba kwa misimu mitano mfululizo tunaishia robo fainali lakini safari hii tunavuka kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu.”