Naibu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, amezindua rasmi jengo la Hazina Ndogo Mkoani Geita, katika hafla iliyofanyika katika Kata ya Bombambili, Manispaa ya Geita.
Uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020, inayolenga kusogeza huduma za serikali karibu na wananchi.
Mhe. Nyongo alisema kuwa kukamilika kwa jengo hilo ni ishara ya dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha utoaji wa huduma serikalini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
“Serikali inatekeleza Ilani kwa vitendo. Jengo hili ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma na kurahisisha huduma kwa wananchi wa Geita” alisema Mhe. Nyongo.
Pamoja na uzinduzi huo, Naibu Waziri aliweka wazi kwamba Wizara ya Fedha itatoa fursa kwa taasisi nyingine za umma ambazo hazina ofisi katika mkoa wa Geita kupata nafasi ya kutoa huduma ndani ya jengo hilo, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.
Elimu ya Fedha kwa Umma na Changamoto ya Mikopo Umiza Katika hotuba yake, Mhe. Nyongo alisisitiza umuhimu wa elimu ya fedha kwa umma, akisema kuwa Wizara ya Fedha inatekeleza mpango wa elimu ya fedha wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26.
Mpango huo unalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya kifedha, hasa katika kuanzisha vikundi vya huduma ndogo za fedha na kupunguza utegemezi wa mikopo isiyo rasmi.
Hata hivyo, alieleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la mikopo umiza inayojulikana kwa majina kama kausha damu, mikopo kuzimia, chuma ulete, na kuonya kuwa mikopo hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi kwa kuwabebesha mzigo wa riba kubwa.
“Natoa wito kwa taasisi zote za kifedha na kamati za ulinzi na usalama kufuatilia suala hili kwa karibu. Hatutavumilia watu wanaotoa mikopo kwa masharti kandamizi na bila vibali rasmi” aliongeza.
Mhe. Nyongo alihimiza wananchi kuwa na nidhamu ya fedha kwa kukopa kwa malengo yenye tija, kama uwekezaji kwenye biashara na uzalishaji mali, badala ya matumizi ya kawaida.
Kwa uzinduzi wa jengo hili jipya la Hazina Ndogo Geita, wananchi wanatarajia huduma bora zaidi za kifedha na maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huo wenye shughuli nyingi za madini na biashara. Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi ya fedha na ulinzi dhidi ya taasisi zisizo rasmi zinazotoa mikopo kwa masharti kandamizi.