
ZAIDI ya wafungwa 100 wa kike walibakwa na kisha kuchomwa moto wakiwa hai wakati wa hali ya machafuko ilipotokea baada ya wafungwa kutoroka gerezani katika mji wa Goma, nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Kwa mujibu wa ripoti mpya kutoka kwa Umoja wa Mataifa, mamia ya wafungwa walitoroka katika gereza la Munzenze Jumatatu iliyopita, baada ya wapiganaji wa kundi la waasi la M23 kuuteka mji huo.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba kati ya wanawake 165 na 167 walivamiwa na kunyanyaswa na wafungwa wa kiume walipovunja gereza. Wengi wa wanawake hao waliuawa baada ya wafungwa hao kuchoma moto jela.
Goma, jiji kubwa lenye zaidi ya watu milioni moja, lilitekwa na kundi la waasi la M23, linaloungwa mkono na Rwanda, lilipovamia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Machafuko yaliyoikumba Goma yalikuwa makubwa, huku miili ya watu ikiwa imetapakaa mitaani na makombora yakiripotiwa kurushwa juu ya nyumba za makazi. Picha za kivunjiko cha jela zilizochukuliwa wiki iliyopita zilionyesha watu wakikimbia kutoka jengo hilo huku moshi ukiwa unapaa angani.
Zaidi ya watu 2,000 waliuawa wakati waasi wa M23 walipokutana na wanajeshi wa Congo, huku Umoja wa Mataifa ukisema takriban watu 900 walipoteza maisha na karibu 3,000 kujeruhiwa.