Mohanmmed Iqbal Dar, aliyebuni jina la taifa la Tanzania, amefariki Dunia akiwa usingizini jijini Birmingham, Uingereza alikokuwa akiishi akiwa na umri wa miaka 80.
Mohammed Iqbal Dar aliyezaliwa Agosti 8, 1944, mjini Tanga, alikuwa mtoto wa Dk Tufail Ahmad Dar, daktari maarufu aliyehudumu katika mikoa ya Tanga na Morogoro nchini Tanzania. Mwaka 1965 alihamia Uingereza alipokuwa akiishi hadi kifo chake.
Igbal alishiriki katika shindano la kutafuta jina la Tanzania lililoandaliwa mwaka 1964 kabla ya Muungano ambako yeye alikuwa mmoja wa wanafunzi 80 walioshindana na hatimaye yeye kuibuka mshindi.
Akizungumzia jinsi alivyobuni jina TANZANIA enzi za uhai wake Iqbal alisema alichukua herufi tatu kutoka jina la nchi ya Tanganyika yaani TAN na kwa upande wa Zanzibar nikachukua herufi tatu za mwanzo ZAN, kisha nikaunganisha nikapata jina TANZAN.
Baada ya hapo alichukua herufi ya kwanza ya jina lake ‘lqbal’ kisha akachukua herufi ya kwanza A ya jina la dini yake yaani Ahmadiya na kuunda jina TANZANIA.
lqbal ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 18 alishinda shindano la kupendekeza jina moja litakalozitaja nchi zote mbili yaani Tanganyika na Zanzibar na kupewa zawadi ya shilingi mia mbili (Tsh 200/=) za wakati huo.