Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde amesema daraja la J.P Magufuli (Kigongo Busisi)KM 3 litaanza kutumika rasmi Aprili 30 mwaka huu.
Hata hivyo, amesema ifikapo Aprili 10, 2025 magari yataanza kupita upande mmoja kwenye daraja hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 97.
Daraja hilo limejengwa kwa lengo la kuunganisha Barabara Kuu ya Usagara – Sengerema Geita KM90 ambayo ni sehemu ya barabara iliyopo kwenye Ushoroba wa Ziwa Victoria inayoanzia Sirari mpakani mwa Tanzania na Kenya hadi Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda.
Kwa sasa sehemu ya barabara hiyo eneo la Kigongo Busisi inaunganishwa kwa kutumia vivuko vikubwa vitatu vya MV Mwanza, MV Misungwi na MV Sengerema.
“Kutokana na idadi kubwa ya magari yanayopita kwa siku, abiria na magari huweza kutumia muda wa takriban saa mbilii kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine hivyo kukamilika kwake kutachochea maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza” amesisitiza Dkt. Msonde.
Amesema baada ya daraja hilo kukamilika, muda wa kuvuka utapungua kufikia wastani wa dakika tatu (3) hadi nne (4) badala ya saa mbili ilivyo sasa.
Akizungumza leo Machi 22, 2025 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma(PIC) ilipokagua ujenzi wa daraja hilo, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Msonde amesema Aprili 10, mwaka huu magari yataruhusiwa kuanza kupita kwenye upande mmoja wa daraja ambao utakuwa umekamilika kwa asilimia 100.
Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3 na upana wa meta 28.45 lina njia mbili za magari zenye upana wa mita 7 kila upande.
Dkt. Msonde amesema daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharimu zaidi Shilingi ya bilioni 610 uimefikia asilimia 97.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Augustine Vuma Holle ameipongeza Wizara ya ujenzi na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kazi waliyoifanya kwenye daraja hilo, huku Kamati hiyo ikibainisha ni miongoni mwa miradi bora iliyoridhisha katika ukaguzi wa kamati hiyo.