RAIS Samia Suluhu Hassan leo anatimiza miaka minne ya uongozi wake wa Awamu ya Sita tangu alipoapishwa Machi 19, 2021 kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kifo cha Dk John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.
Wakati anahutubia Bunge la Tanzania mwezi mmoja baadaye jijini Dodoma, Rais Samia aliahidi kwamba ataendeleza mema yaliyofanywa na mtangulizi wake, Dk Magufuli.
Pia, alisema atasimamia na kuendeleza mengine ambayo uongozi wake wa Awamu ya Sita utakuwa umeyaanzisha.
Leo hii tunapoadhimisha miaka minne ya uongozi wake katika nafasi hii ya juu ya madaraka ya nchi, hakuna shaka yoyote, Rais Samia ameyaishi maneno yake.
Ametekeleza aliyoahidi na amefanya makubwa zaidi kwa ustawi wa nchi.
Toleo la leo limebeba sauti nyingi za Watanzania kuhusu mambo yaliyofanywa na Rais Samia ambayo yameleta mafanikio makubwa kwa maendeleo ya Tanzania na watu wake kuanzia katika huduma za jamii hadi katika diplomasia ya uchumi.
Chini ya Rais Samia, serikali imeboresha huduma za jamii zikiwamo za afya, elimu, maji na kupunguza umasikini, ambako kwa mujibu wake umasikini umepunguzwa kwa kiwango cha asilimia 26 kutoka katika kiwango kilichokuwapo mwaka 2015.
Kwa mfano, katika sekta ya afya, serikali imeongeza miundombinu, vifaa tiba na upatikanaji wa dawa.
Kwenye elimu, ukiacha majengo mazuri ya madarasa na maabara yaliyojengwa kote nchini, mikopo na wanufaika wa elimu ya juu wameongezeka, usajili katika shule za msingi na sekondari umeongezeka na udahili umeongezeka katika vyuo vikuu.
Katika sekta ya maji, Tanzania imefikia mafanikio ya Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs), ikitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 – 2025 ambayo sasa imefikisha maji vijijini kwa asilimia 80 na mijini asilimia 90 na wakati malengo ya ilani ni asilimia 85 na 95 mtawalia.
Ni imani yetu kuwa kazi hii kubwa iliyofanywa na Rais Samia katika miaka minne ya uongozi wake inaakisi maono yake chini ya falsafa yake ya ‘4R’ ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya Taifa.
Kubwa ni Watanzania kuendelea kumuunga mkono, Rais Samia na serikali yake ili aendelee kuwapatia maendeleo zaidi.
Na hapa ni lazima kusisitiza amani na utulivu udumishwe nchini ili haya yanayofanywa sasa yaendelea kutekelezwa. Rais Samia amethubutu, ameweza na anasonga mbele. Kazi Iendelee!