
Rais Donald Trump ametia saini amri ya utendaji inayoiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, akiituhumu kwa “vitendo vinavyokiuka sheria na visivyo na msingi vinavyoilenga Marekani na mshirika wetu wa karibu Israel”.
Hatua hiyo inaiwekea vikwazo vya kifedha na visa kwa watu binafsi na familia zao wanaosaidia katika uchunguzi wa ICC wa raia au washirika wa Marekani.
Trump alitia saini hatua hiyo wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipokuwa akizuru Washington.
Novemba mwaka jana, ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita huko Gaza, jambo ambalo Israel inakanusha. ICC pia ilitoa kibali cha kukamatwa kwa kamanda wa Hamas.
Amri ya utendaji ya Trump ilisema hatua za hivi majuzi za ICC “ziliweka historia ya hatari” ambayo inahatarisha Wamarekani kwa kuwaweka kwenye “unyanyasaji na uwezekano wa kukamatwa”.
“Tabia hii mbovu nayo inatishia kukiuka uhuru wa Marekani na inadhoofisha kazi muhimu ya usalama wa kitaifa na sera ya kigeni ya serikali ya Marekani na washirika wetu, ikiwa ni pamoja na Israel,” amri hiyo ilisema.
Marekani si mwanachama wa ICC na mara kwa mara imekataa mamlaka yoyote ya chombo hicho juu ya maafisa wa Marekani au raia.
Chanzo: BBC Swahili