MTWARA: JAMII katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara hususani wanaume wanaoishi na wanawake wenye fani mbalimbali ikiwemo ufundi chuma, wameshauri kuwaruhusu wanawake hao waendeleze fani hiyo ili waweze kuwa mafundi kama ilivyokuwa mafundi wengine.
Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa mafunzo ya wiki mbili yanayoendelea kwa vijana wa fani hiyo kuhusu masuala ya ufundi chuma, Mwenzeshaji wa mafunzo hayo Omari Mohamed amesema baadhi ya wanawake hao wengi wao wamekuwa wakipitia changamoto hiyo na kupelekea kushindwa kuendeleza fani hiyo.
Mafunzo hayo yamefanyika katika manispaa hiyo na kukutanisha vijana wa kike na wa kiume wa fani hiyo yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala mbalimbali ya sanaa na utamaduni la ADEA lililopo kwenye manispaa hiyo, yanayofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
‘’Unakuta mwanafunzi wa kike anapitia haya mafunzo mwisho wa siku anashindwa kuendeleza fani anabaki nyumbani na wengi wao wanashawishiwa, sasa sijajua kama na wanaume au lah……unakuta mwanamke mwingine hii kazi anaitaka kwa kuwa ndiyo fani aliyochangua na kuolewa anataka kwahiyo changamoto inakuja hapo’’amesema Mohamed
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo la ADEA, Saidi Chilumba amesema fani hiyo imekuwa ngumu kwasababu baadhi ya jamii inaamini kuwa fani hiyo ni ya watoto wa kiume pekee lakini mafunzo hayo yameshirikisha vijana wa jinsia zote ambao wamejifunza kwa nadharia pamoja na vitendo kwa kutengeneza vitu mbalimbali vya chuma.
Hata hivyo amewataka vijana hao kubuni bidhaa zitazokuwa na uwezo wa kuwauzia wananchi wa kawaida ambavyo ni vidogo vidogo vinavyohatajika na jamii ila hawajuwi wapi vinapatikana hivyo ni fursa kubwa kwao na maamuzi ya kushirikisha vijana hao wa kike ni kutokana vile wanapata mafunzo lakini hawaonekani mitaani wakiendelea fani hiyo.
Baadhi ya vijana hao wa kike akiwemo Asfa Rashidi mkazi wa magomeni kwenye manispa hiyo ‘’Sisi watoto wa kike kwa hii fani tunapokuja mtaani tatizo jamii inatukatisha tamaa, tunaambiwa mnafanyaje hizi kazi za watoto wa kiume au unatokaje nyumbani mtoto wa kike kutwa mzima unaenda kushinda kijiweni, basi unasema ngoja niachane tu na hii kazi’’






