BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya Sh bilioni 32,517,899,127 ambapo halmashauri hiyo imekisia kukusanya na kutumia fedha hizo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Hayo yamejiri wakati wa kikao hicho cha baraza hilo la madiwani hao kilichofanyika kwenye halmashauri hiyo.
Akichangia mada katika kikao, Diwani wa Viti Maalumu, Mariam Lilepe ameipongeza rasimu hiyo ya bajeti na kuhusu kutilia mkazo suala la ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao mbalimbali yanayozalishwa kwenye halmashauri ili kukuza pato la halmashauri.
Hata hivyo amesisitiza suala la ujenzi wa eneo la kupaki magari (Parking) kwenye halmashauri hali itayochangia tija zaidi kwenye ukusanyaji wa mapato hayo.
Diwani wa Kata ya Mayanga, Arif Premji ameunga mkono suala hilo la ujenzi wa ghala ambapo ameliomba baraza hilo kuwa, ujenzi huo ufanyike kwenye kata hiyo kwasababu ni moja ya kata inayochangia pato la halmashauri.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya amepongeza mchakato mzima wa rasimu hiyo ya bajeti kwasababu imezingatia maeneo yote muhimu ikiwemo sekta ya elimu na mengine.
Mbali na hilo Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza suala la utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuwa itolewe kabla ya Februari 2025 kumalizika.
“Hakikisheni mnatoa mikopo hii kabla mwezi huu wa 2/2025 haujaisha, kwasababu pesa tayari ipo”amemsisitiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo.

