BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara limepitisha makadirio ya bajeti ya Sh bilioni 40.239 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Hayo yamejiri leo wakati wa kikao maalum cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kuhusu makisio ya mpango wa bajeti kwa mwaka huo wa fedha 2025/2026, kilichofanyika kwenye halmashauri hiyo.
Akiwasilisha bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya Wilaya ya Tandahimba, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wilayani humo David Sinyanya alisema katika bajeti hiyo ni kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo Sh bilioni 7.3 mapato ya ndani, Sh bilioni 24.9 ruzuku ya mishahara, Sh bilioni 5.06 wafadhili na Sh bilioni 2.8 matumizi mengineyo (OC).
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji DCI Mariam Mwanzalima alisema kila mwaka wa fedha wamekuwa na jitihada ya kuhakikisha wanakamilisha miradi ya nyuma ili waweze kwenda na miradi mipya na ili waweze kufikia malengo ya makusanyo hayo ni imani yake kwa ushirikiano na wananchi wake wataweza kufikia malengo hayo.
Hata hivyo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 halmashauri ilikisia kukusanya Sh bilioni 6.1 lakini hadi kufikia Disemba 2024 ilikusanya Sh bilioni 6.9 sawa na asilimia 112.
Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Michael Mntenjele kupitia baraza hilo amesisitiza suala la hali ya ulinzi na usalama katika wilaya hiyo kuwa ni salama kwani vikosi vyao vinaendelea na majukumu yake kama kawaida.
“Ila na sisi wananchi tunapaswa kutimiza majukumu yetu ya ulinzi shirikishi ili kuendelea kudumisha hali ya amani katika maeneo yetu”alisema Mntenjele
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Baisa Baisa ameendelea kuwaomba madiwani hao pamoja na watendaji wa halmashauri kwa ujumla kuwa, waendelee kushirikiana katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ili waweze kufikia malengo husika ya bajeti hiyo ya mwaka 2025/2026 kama ilivyokuwa bajeti za miaka iliyopita.



