BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya Sh bilioni 33,544,971,406 ambapo manispaa hiyo imekisia kukusanya na kutumia fedha hizo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumza wakati wa kikao cha baraza la madiwani hao, Meya wa manispaa hiyo Shadida Ndile amesema madiwani hao waende wakawahamasishe wananchi wao wakakusanye fedha ili waweze kuyatekeleza yale wanayotamani kuyaona yanayoendelea kwenye maeneo yao.
Aidha amewasisitiza madiwani hao wazingatie vipaumbele ambavyo kila kata vimeweka “Naamini kata zote tumezigusa kwenye miradi ya maendeleo na dhamira yetu ni kuendelea kugusa miradi ya maendeleo ili kipunguza changamoto kwa wananchi”amesema Ndile
Ameongeza kuwa, ” Twende tukakusanye tukirudi tutaangalia kila kata kipaumbele chake upande wa elimu kipi, afya, mazingira kipi tutakwenda kuyafanya lakini haya yote yanawezekana endapo tutakuwa na fedha za kutosha tutazoweza kwenda kutekeleza majukumu haya”
Hata hivyo amewashukuru wataalamu katika manispaa hiyo kwa kuchakata vizuri mpango huo wa bajeti uliyopitishwa na madiwani hao hivyo ni imani yake kuwa baina ya timu hizi mbili wakienda kushirikiana wataenda kupunguza baadhi ya changamoto.
Diwani wa Kata ya Naliendele, Masudi Dali kupitia kikao hicho ameunga mkono bajeti hiyo na kwamba madiwani hao waendelee na ukusanyaji mapato katika maeneo yao ili waweze kufikia malengo yanayokusudiwa.
Diwani wa Kata ya Shangani, Abuu Mohamed ameliomba baraza hilo kuangalia suala la kuwapatia mikataba wafanyabiashara wa soko la kiyangu (Sokosela) lililopo kwenye manispaa hiyo ili waweze kufanya kazi zao kwa uhakika.


