NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dk. Hussein Mohamed ameiagiza Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kuendelea kuhamasisha wawekezaji ili waje kuwekeza katika kongani ya viwanda inayojengwa kijiji cha maranje Halmashauri ya Mji Nanyamba Wilaya ya Mtwara mkoani mtwara.
Akizungumza mkoani Mtwara alipotembelea kongani hiyo ya viwanda inayojengwa kwenye kijiji hicho cha maranje, Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo, amesema serikali pekee haiwezi kuendelesha kongani hiyo hivyo wanahitaji uwekezaji kutoka sekta binafsi ambao wako tayari.
‘’Lengo la serikali ifikapo mwaka 2030 asilimia 100 ya korosho inayozalishwa nchini yote ibanguliwe nchini, maana yake ni lazima tuwe na viwanda vya kutosha vya kubangua nchini na hii siyo korosho peke yake na ufuta pia kwahiyo lazima tuwe na hivi viwanda vya kuongeza thamani’’amesema Hussein
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Mangile Malegesi amesema eneo lote hilo la kongani lina jumla ya hekari 1572 elfu linalotarajiwa kuwa viwanda zaidi ya 60 ambapo litagharimu takribani Sh bilioni 5.6 hadi kukamilika kwa mchakato huo mzima wa ujenzi.
‘’Kukamalika kwa maradi huu tunatarajia sasa kwa mkoa huu wa mtwara na ukanda mzima wa kusini uchangamke zaidi kwani ajira zitakazopatiakana hapa hazitahusisha watu wa mtwara pekee bali hata kutoka nje ya mkoa na sehemu kubwa ni akina mama na vijana na ajira zitapatikana nyingi zaidi katika eneo letu hili la maranje’’
Hata hivyo amezitaja faida mbalimbali zitazotokana na kongani hiyo ikiwemo ajira za kawaida takribani 35 elfu kwa watu wataopata ajira za moja kwa moja, uuzaji wa korosho na bidhaa zake badala ya kuuza tu korosho ghafi kama vile ganda lenyewe.
Hata hivo mafuta yanayotokana na ganda la korosho na zingine ‘’Kwahiyo mkulima ataenda kunufaika na zao lake mara mbili ya kile anachokipata na serikali itapata mapato ya kutosha kwasababu ile tozo aliyokuwa anaipata kwenye korosho ghafi sasa itapata mapato yanayozalishwa na viwanda’’
Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu huyo, ametembelea katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) Naliendele na akiwa katika taasisi hiyo amesema lengo la serikali hadi kufikia mwaka 2050 nchi iweze kufikia uchumi wa kati wa juu na ili kufikia hapo, moja ya sekta ya mageuzi ikiwemo sekta ya kilimo.
‘’Ili ufanikiwe kwenye kilimo, hakuna kilimo bila utafiti kwahiyo TARI mtakuwa sehemu kubwa muhimu ya mageuzi ya nchi hii kiuchumi kupitia utafiti na serikali imeahinisha mazao kumi na tano na korosho ni miongoni mwa mazao hayo, tunataka tufikie uzalishaji wa tani milioni 1 ifikapo 2030 na TARI Naliendele mna nafasi kubw mno eitha kutuangamiza au kutunyanyua’’amesema Hussein





