Viongozi wa dini mbalimbali (Interfaith) mkoani Mtwara wametakiwa kuendelea kuwaelimisha wananchi katika masuala mbalimbali ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025 hasa suala la amani na utulivu.
Hayo yamejiri wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa viongozi wa dini mbalimbali mkoani humo kuhusu elimu ya uraia yanayoendeshwa na Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) yaliyofanyika kwenye Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padre Charles Kitima amesema viongozi hao dini wakati wakiendelea na shughuli za kuabudu wasiache kuwaelimisha wananchi hao masuala ya kisiasa ila jambo la msingi waangalie mazingira ya kutoa elimu hiyo.
“Ni haki yako kiongozi wa dini kuwaambia wananchi masuala ya siasa ila angalieni namna ya kuongelea masuala haya ili waweze kukuelewa na waweze kujiandaa na mambo ya uchaguzi, tuwape watu elimu ya uchaguzi wenye amani na utulivu,”amesema Kitima
Aidha lengo la mafunzo hayo ni kuwapatia viongozi hao wa dini baadhi ya mambo muhimu wanayopaswa kuzingatia katika uongozi ikiwemo maarifa, uelewa juu ya masuala ya kuongoza nchi, kujipatia nyenzo za kutawala na kuongoza pamoja na namna ya kufata taratibu.
“Viongozi wa kisiasa wameumbwa kuwatumikia wanadamu wote waliyoumbwa kwa mfano wa Mwenyezi Mungu, wanaojituma, wanaojielewa na kiongozi wa kisiasa ni agizo la Mwenyezi Mungu hivyo twendeni tukatoe elimu ya masuala haya ya uchaguzi kikamilifu ili wananchi wapate uelewa “amesisitiza Kitima.
Amesema wanahitaji elimu ya uraia nchini iwe endelevu katika jamii hivyo viongozi hao wa dini waje na mkakati wa kuona elimu hiyo kuwa ni sehemu ya wajibu wao ili mwisho wa siku wawe na Taifa lenye uadilifu.
Hata hivyo kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameendelea kuwakumbusha viongozi hao kuwa hawapaswi kufungamana na chama chochote kike cha siasa pia wawaambie wananchi wajitokeze kupiga kura wakati uchaguzi huo utakapofika hivyo wanao wajibu wa kujiandaa kikamilifu na kushiriki moja kwa moja katika zoezi hilo.
Mkurugenzi wa Miradi wa TEC, Padre Chrisantus Ndaga amewataka viongozi hao wanapojiandaa na uchaguzi mkuu huo kuhakikisha wanaendelea kujenga uelewa zaidi hasa katika masuala hayo ya uchaguzi ili kuwafanya watu wafanye maamuzi sahihi katika ushiriki wao kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.
Viongozi hao wa dini waliyopatiwa mafunzo hayo wakiwemo kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani Mtwara, Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).